Mwasiti: Najipanga kusaka elimu (original) (raw)

Muktasari:

“Nimejipanga kuingia kwenye elimu. Kuna mambo mengi tunayoweza kufanya kama wasanii katika kuhakikisha tunainua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi, kwa muda mrefu nimetoa elimu kwa jamii na sasa ni muda wa kukuza elimu nchini,”

Dar. Mwimbaji wa zouk nchini Mwasiti Almas amesema mwaka huu amejipanga kutumia muda wake mwingi kuwekeza katika elimu ili kuinua ufaulu kwa wanafunzi wa sekondari.

Akizungumza na Mwananchi jana alisema amefanikiwa kusambaza elimu kupitia kazi zake za muziki, lakini sasa ana mpango wa kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinapanda.

“Nimejipanga kuingia kwenye elimu. Kuna mambo mengi tunayoweza kufanya kama wasanii katika kuhakikisha tunainua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi, kwa muda mrefu nimetoa elimu kwa jamii na sasa ni muda wa kukuza elimu nchini,”

Mwasiti anayetamba na wimbo wa ‘Mapito’ aliomshirikisha Ali Nipishe anasema sanaa ya muziki hivi sasa inalipa. Hivyo ni wajibu wa wasanii kurudisha fadhira kwa jamii na kufanya kazi za kujitolea.

Akizungumzia suala la ukimya wake katika fani Mwasiti anasema “Nashangaa baadhi ya watu wanasema nimepotea na wengine nimefunikwa na chipukizi wa kike, si kweli ila kila kipya kinapotokeza machoni pa watu huwekewa umakini zaidi kuliko cha zamani,” alifafanua.

Mwimbaji huyo zao la THT hivi karibuni anatarajia kutoa wimbo mpya alioshirikiana na mtayarishaji wa muziki Tudd Thomas uliotengenezwa katika Studio za Saround Town. Kwa mujibu wa Mwasiti wimbo huo bado hajaupa jina na anatarajia kuuweka hadharani mwezi wa sita, huku wimbo wake wa Mapito nao akiwa ameutoa mwezi wa sita.