uchunguzi | (original) (raw)
TUFUFUE UANDISHI WA HABARI WENYE TIJA
Na Tumbi Kiganja
Dodoma. Waandishi wa habari wametakiwa kufufua uandishi wa habari makini, habari za uchunguzi na zenye kuhamasisha mabadiliko kwenye jamii. Hayo yalisemwa na wadau mbalimbali kwenye mjadala maalumu wa kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari Duniani (WPFD) yanayoadhimishwa kila Mei 3 ya mwaka.
Majadiliano hayo yaliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), na kufanyika Mei 2, 2024 Jijini Dodoma na kujadiliana pamoja na mambo mengine kuhusu Sheria na Sera za habari, hali za kiuchumi za waandishi na vyombo vya habari, pamoja na masuala ya jinsia na usalama wa waandishi wa habari. Hii ikiwa ni mwendelezo ya maadhimisho ya WPFD mwaka 2024 yaliyoanza Mei 1, 2024 na kuhitiishwa Mei 3 2024.
Mara baada ya majadiliano hayo, wadau walitoka na maadhimio kadhaa ambayo wanaamini yakifanyiwa kazi basi yataleta mabadiliko makubwa katika tasnia ya habari nchi. Maadhimio ni pamoja na kufufua uandishi wa habari makini wa habari za uchunguzi wenye kuangazia mahitaji ya jamii.
Pia, kuusukuma uongozi wa kisiasa kwa ujasiri uweze kuona umuhimu wa kuweka mazingira huru zaidi ya kufanya kazi kwa kufanya marekebisho ya sheria zinazoathiri tasnia ya habari
Washiriki walikubaliana pia iwapo kuna nia ya dhati ya kuzingatia misingi ya demokrasia, serikali iangalie upya sheria ya takwimu kuhusiana na kufanya utafiti kwani inakwaza waandishi wa habari kufanya utafiti kwa uhuru ili kuwasaidia wananchi na taifa kwa ujumla. Serikali iingilie kati kuwataka wamiliki wa vyombo vya habari wazingatie sheria za kazi kwa kuwalipa mishahara wafanyakazi na haki zao zingine kama mikataba ya kazi, bima, NSSF.
Maazimio mengine ni pamoja na waandishi wa habari na taasisi za kihabari. Kuiangalia tena sheria ya huduma ya vyombo vya habari ili ikidhi manufaa ya uandishi uliotukuka kwa manufaa ya wananchi.
Kuna haja ya kuangalia mchango wa vyombo vya habari katika uchumi wa nchi ili kuamsha ari kwa serikali kutambua umuhimu wa vyombi vya habari pamoja na kuwajengea uwezo waandishi, wahariri na meneja wa vyombo vya habari kujitambua ili wawe sehemu ya kuleta mabadiliko na kurejesha heshima iliyopotea ya tasnia ya habari nchini.
Awali, akitoa neno la ufunguzi, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura alisema kuwa majadiliano haya ni mahsusi ili kufanya tathmini kuhusu mazingira ya kazi ya mwandishi wa habari nchini Tanzania, kutathmini mifumo ya kisheria, sera na kitaasisi inayodhibiti tasnia ya habari pamoja na kutathmini matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yaliyoripotiwa katika vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Jenerali Uliumwengu ambaye alikuwa mgeni rasmi wa majadiliano hayo alisema kuwa mazingira ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari yamekuwa na changamoto tangu enzi za chama kimoja ingawa waandishi wa kipindi hizo waliweza kufanya kazi bila ya uwoga na kufuata isingi ya kitaaluma.
“Zamani kulikuwa na vyombo vya habari vichache, vya serikali na chama hivyo waandishi walipaswa kuandika kwa kufuata misimamo ya chama na serikali. Mambo yalianza kubadilika miaka ya 90 baada ya kuwa na uhuru wa kisiasa na kupelekea kufunguliwa kwa vituo vingi vya redio, runinga na magazeti”, alisema Ulimwengu.
Aidha Ulimwengu alizungumzia kwa ujumla hali ilivyokuwa kabla ya uhuru, baada na sasa.
Majadiliano hayo pia yalihusisha mwandishi mkongwe Salim Salim ambae alizungumzia kuhusu usalama na ulinzi wa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) – Mussa Juma, pamoja na Wakili James Marenga aliyezungumzia masuala ya Sheria na Sera za habari nchini.