Andres Iniesta: Kipi kifuatacho kwa gwiji wa soka baada ya kustaafu? - BBC News Swahili (original) (raw)
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Andres Iniesta alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya mara nne akiwa na Barcelona
12 Novemba 2024
Kuna wachezaji kadhaa wameshinda mataji ya 'Utatu Mtakatifu' katika kandanda - Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Mataifa ya Ulaya na Kombe la Dunia - lakini Iniesta anaonekana kuwa mchezaji pekee aliyeshinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika fainali za mashindano yote matatu.
Mchezaji huyo kutoka Fuentealbilla, kijiji kidogo katika jimbo la Albacete mashariki mwa Uhispania, alistaafu soka akiwa na umri wa miaka 40 mwezi Oktoba.
Pia unaweza kusoma
Mafanikio yake
Safari yake ya soka ilimtoa kaskazini mwa Albacete hadi Barcelona, umbali wa saa tano na nusu kwa gari, akiwa mvulana mwenye haya, anayetamani nyumbani, wakati huo akiwa na umri wa miaka 12, hadi kuwa mwanasoka aliyependwa Uhispania na kushinda mataji 35, ikijumuisha mataji matatu katika msimu mmoja, mara mbili akiwa na Barcelona. Mataji tisa ya La Liga, manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia na mawili ya Mataifa ya Ulaya.
Mwaka 1999, akiwa nahodha wa Barcelona katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 15, Iniesta alifunga bao la ushindi katika Kombe la Primia la Nike.
Robo karne baadaye, nampata akiwa Dubai, makazi yake ya sasa baada ya kucheza misimu sita akiwa na klabu ya Vissel Kobe ya Japan na kisha kucheza katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambako amecheza msimu huu na sasa anapanga kuwa kocha.
Makocha wengi wakubwa (Pep Guardiola, Luis Enrique, Luis Aragones, Louis van Gaalna V icente del Bosque) walisaidia kuuboresha uwezo wa Iniesta kama mchezaji, kwa namna tofauti.
Lakini Iniesta anahitimisha kwamba jambo moja ambalo wote walikuwa wanafanana ni "ni akili zao za kuvutia kuhusu soka, kwa sababu wote walikuwa bora.”
Alama ya kitaifa
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rafiki wa Iniesta, Dani Jarque alifariki kutokana na mshtuko wa moyo 2009
Safari yake katika soka haikuja bila gharama, kwake binafsi na kwa kazi yake. Kifo cha rafiki yake mkubwa Dani Jarque kutokana na mshtuko wa moyo, akiwa na umri wa miaka 26, alipokuwa akizungumza na mpenzi wake kwa simu kutoka kwenye chumba chake cha hoteli cha Florence wakati wa kambi ya mazoezi ya kabla ya msimu mpya wa Espanyol mwaka 2009.
Kisha majeraha ya muda mrefu kabla ya Kombe la Dunia la 2010, yalimtumbukiza katika dimbwi la huzuni ambayo iliathiri sana maisha yake na kutishia kuharibu kazi yake.
Kwa ushauri nasaha na upendo na uungwaji mkono kutoka kwa walio karibu naye, na upendo wa mke wake mpendwa Anna Ortiz, yote hayo yalisaidia kumwondoa katika giza.
Na ushindi katika fainali ya Kombe la Dunia 2010 dhidi ya Uholanzi, pia ulimsaidia kumpa faraja katika uchezaji wake na kwa timu ya taifa.
Maandishi yaliyoandikwa kwa mkono kwa ajili ya rafiki yake – akiwa amevalia fulana lake - "Dani Jarque - siempre con nosotros [daima uko nasi]" ambayo aliyafichua baada ya kufunga – yatakumbukwa kama mojawapo ya matukio ya kugusa na ya kuvutia katika soka.
Nini kinafuata kwa Iniesta?
Kustaafu sasa kunaweza kumruhusu kutumia muda wake mwingi na mkewe Anna, ambaye walianza kuchumbiana mwaka 2008 kabla ya kufunga ndoa mwaka 2012, wana mabinti watatu na wavulana wawili.
Mwaka 2014, wana ndoa hao walipoteza mtoto ambaye hajazaliwa kwa sababu ya kuharibika kwa mimba.
Kustaafu pia kutampa muda zaidi na klabu yake ya soka ya Albacete Balompie, ambayo ameisaidia kifedha kwa zaidi ya mara moja.
Kwa sasa anaishi Dubai, Iniesta anasema: "Mpango wangu ni kuacha kucheza soka, nibaki hapa UAE. Na nimeanza kozi ya kuwa meneja.
"Maisha yangu yote nimekuwa nikifikiria kama mchezaji, lakini sasa ninapaswa kufikiria kwa namna nyingine. Ni ulimwengu mpya. Sio mpya tu, lakini kuna mambo mengi mapya ya kujifunza.
"Ni sawa na nilipoanza kucheza soka - nilichotaka kufanya ni kujifunza, na kadiri nilivyojifunza, ndivyo nilivyozidi kuwa bora. Sasa nitajaribu kufanya vivyo hivyo [kama meneja]."
Iniesta amekuwa mwanasoka bora. Kwa maneno yake mwenyewe, anasema cha muhimu "zaidi ya kushindana, kwa ajili ya timu yako au bendera yako, ni kuwa na ubinadamu na mtu mzuri."
Iwe uwanjani, kwenye chumba cha mikutano au popote anapochagua kuishi maisha yake mapya. Kwa hakika bado hatujausikia mwisho wa Andres Iniesta.
Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi