EPL: Pale ambapo Man United ilikosea dhidi ya Tottenham Hotspurs - BBC News Swahili (original) (raw)

,

Chanzo cha picha, Getty Images

30 Septemba 2024

Siku zote nadhani jambo rahisi zaidi ambalo meneja anaweza kufanya katika soka ni kuchagua na kupanga timu ambayo ni thabiti na itakupa kila kitu - lakini hilo si rahisi kwa mkufunzi wa Manchester United Erik ten Hag kwa sasa.

United walikuwa wakicheza vibaya walipopata mpira kipindi cha kwanza katika mechi waliolazwa 3-0 nyumbani dhidi ya Tottenham Jumapili, lakini pia walicheza vibaya zaidi walipokosa mpira - na hilo linapaswa kuwa wasiwasi mkubwa zaidi.

Nilishangaa sana wakati Ten Hag alipotoka sare ya Jumatano ya Ligi ya Europa dhidi ya Twente na kukubaliana kwamba klabu hiyo ya Uholanzi "ilikuwa na ari zaidi" na nilidhani kungekuwa na mabadiliko makubwa katika mchezo dhidi ya Spurs.

Ten Hag kimsingi alikuwa akiwaambia wachezaji wake kwamba hali yao ya kutokuwa na ari lazima ibadilike, na kwamba mambo yalitakikana kubadilika wikendi... lakini hilo halikufanikiwa .

Kidogo nilichotarajia dhidi ya Tottenham kilikuwa ni kikosi cha United kilichosisimka lakini mawazo hayo yalikosekana mwanzoni mwa mchezo, na mambo yakazidi kuwa mabaya zaidi.

Pia unaweza kusoma

'Hakuna shinikizo isio na madhara'

.

Chanzo cha picha, BBC

Ninapotazama United, naweza kuona kile ambacho Ten Hag anajaribu kufanya wakati timu yake inamiliki mpira, lakini wanachofanya wakati hawana mpira ni muhimu vile vile.

Kwa hilo, ninamaanisha jinsi walivyojipanga, na jinsi wanavyolinda lango lao.

Watu wakati mwingine huchanganya juhudi na matumizi hayo kwa kucheza mbinu ya kushinikiza, lakini timu inaweza kucheza vyovyote vile na bado kuwa na dhamira na ari ya kutaka kushinda.

Kwa hivyo sio rahisi kusema United ilibabaika dhidi ya Spurs kwa sababu hawakuwa na msukumo au kukimbia kila mahali. Hawakuambiwa kufanya hivyo, lakini hiyo yenyewe isingekuwa shida ikiwa ndivyo walivyotaka kucheza.

Walianza na Bruno Fernandes na Joshua Zirkzee kama washambuliaji wawili waliocheza nambari 10, na wakawataka kujaza nafasi ya kiungo cha kati ili wasitawaliwe katikati ya uwanja.

Kwa kufanya hivyo, walipeana mpira kwa walinzi wa Tottenham kwa urahisi .

.

Kuandaliwa ili kuwa tayari kukabiliana na upinzani si lazima kuutafuta mpira na kuwaweka katika shinikizo kali mabeki wa Spurs .

Badala yake, ni kupigania na hatimaye kushinda mipira ya juu, kuwakaba wanaosubiri kupewa pasi na kutoruhusu wachezaji wa upinzani kuwapita mbali kubaini hatari - hata ikiwa iko eneo la lango lenu .

Mbinu waliotumia United ilimaanisha kwamba pia wangeweza kuwasukuma wapinzani wao mara kwa mara, kama vile katika wingi wakati kipa wa Spurs Guglielmo Vicario alipokuwa akipiga mpira, lakini wazo lilikuwa kwamba katika uchezaji wa jumla ilikuwa vigumu zaidi kuwapita .

Hilo lilidumu chini ya dakika tatu, kwa sababu bao la kwanza walilofungwa lilikuwa la kipuuzi.

Ulikuwa mchezo mzuri sana wa Micky van de Ven, lakini hakukuwa na jinsi angeweza kufika mbali hivyo uwanjani bila kukabiliwa au hata kuchezewa visivyo.

Ilikuwa ni kasi ya ajabu na nguvu, si ustadi wa ajabu, na Van de Ven alikimbia kupitia mapengo makubwa huku akimzima Diogo Dalot na kupiga krosi safi iliofungwa na Brennan Johnson.

Baada ya kufungwa bao 1-0, United walikuwa wakipoteza mipira, wakipoteza makabiliano, na kufanya mchezo kuwa mgumu upande wao.

Hawakuwa wakiwafuatilia wapinzani na hawakujua nani wa kumkaba.

Kwa kifupi, walikuwa wamevurugwa.

Tottenham wangeweza kuwa kifua mbele kwa mabao 3-0 wakati Bruno Fernandes alipotolewa kwa kadi nyekundu kabla ya muda wa mapumziko - uamuzi ambao ulikuwa mkali na mechi ingekuwa imekamilika .

Meneja wa Spurs Ange Postecoglou amekuwa akikosolewa kwa kuwa jasiri sana katika baadhi ya mbinu zake, lakini timu yake inajaribu kushinda mechi kwa kucheza soka la kusisimua mbele ya uwanja, na dhidi ya United ,mbinu yao ilifua dafu.

Walianza vyema kwa kusonga mbele na mpira kutoka katikati, na sababu mojawapo ya Spurs kutawala kipindi cha kwanza ni kwamba walikuwa wanajiamini sana katika kile walichokuwa wakijaribu kukifanya.

United walikuwa na mpango pia, lakini walilazimika kucheza bila ya mshambuliaji Rasmus Hojlund, ambaye ndiye mshambuliaji wa kipekee waliye naye. Aliingia mwishoni mwa mchezo dhidi ya Spurs lakini hayuko sawa baada ya jeraha la misuli ya paja.

Walitumia namba 10 wawili kama walivyofanya Jumapili iliyopita na kufanikiwa, wakicheza kwenye mashambulizi ya kaunta na kutumia mawinga wao wa kasi.

Iliwapa nafasi kadhaa dhidi ya Spurs pia, ingawa hawakuwa wakicheza vizuri, hivyo itakuwa ngumu kusema hawana mapango au walionekana wanababaika wakiwa na mpira.

Badala yake, tofauti na Spurs, nadhani kutojiamini katika mifumo yao ya uchezaji ndio suala lao kuu wanapocheza kutoka nyuma.

Hiyo pia imesababishwa na ukweli kwamba United imekuwa ikibadilisha timu kila mara - wachezaji wao wa kati Matthijs de Ligt na Lisandro Martinez walikuwa wameshirikiana mara tatu pekee kabla ya Jumapili, kwa mfano.

Kwa kweli nadhani upande huo wa mambo utaimarika kadri wachezaji wao wanavyozoeana, kwa sababu tunajua ni wachezaji wazuri.

Spurs walizawadiwa kwa ujasiri wao

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni jinsi timu inavyochukulia kila mechi ndivyo inanitia wasiwasi zaidi.

Huwezi kuwa na ujasiri unaohitaji kucheza kupitia mawinga na kuleta mpira kutoka nyuma ikiwa daima una wasiwasi sana kuhusu kufungwa.

Vitendo wanavyopaswa kufanya bila mpira ndio msingi wa kile wanachofanya wanapoupata na, hivyobasi iwapo hataweza kutawala mpira hawatafanikiwa kwa hilo pia.

Ten Hag alibadilisha mbinu katika kipindi cha pili dhidi ya Spurs, huku United ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, alipowaleta Casemiro na Mason Mount.

Kulikuwa na kipindi ambapo wachezaji wa kati wa United walikuwa wakifika nusu ya mstari na kuwaweka Dominic Solanke na James Maddison chini ya shinikizo, na iliipa United jukwaa la kutengeneza nafasi nyingi zaidi.

Kila mtu alikuwa akipigana kwa bidii kwa sababu hawakuwa na cha kupoteza, kwa hivyo inawezekana - lakini ari hiyo yote ilikuwa wapi wakati walipokuwa wachezaji 11 dhidi ya 11?

Hilo ndilo swali Ten Hag anapaswa kuwauliza wachezaji wake wiki hii.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah