Guardiola asema amechochewa na ushindani mkubwa wa Arsenal - BBC News Swahili (original) (raw)

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pep Guardiola (kushoto) na mwenzake wa Arsenal Mikel Arteta walifanya kazi pamoja kwa miaka mitatu na nusu hadi Desemba 2019.

28 Septemba 2024

Mkufunzi wa Manchester City Pep Guardiola amesema amechochewa na ushindani mkali zaidi na Arsenal huku athari zake zikiendelea kujitotokeza kutokana na mechi yao la Ligi Kuu ya Uingereza kwenye Uwanja wa Etihad wikendi iliyopita.

Sare ya Jumapili ya 2-2 kati ya wapinzani wa taji ilishuhudia mambo mengi, akiwemo mshambuliaji wa City Erling Haaland akirusha mpira kichwani mwa beki wa Gunners Gabriel.

Kufuatia mechi hiyo, wachezaji wa City John Stones na Kyle Walker walisema The Gunners walitumia "muujiza" huku wakijaribu kulinda uongozi wao wa 2-1 kipindi cha mapumziko.

Stones aliyeingia uwanjani kama mchezaji mbadala aliambulia kusawazisha katika dakika ya nane ya muda ulioongezwa.

Akizungumza siku ya Ijumaa, Guardiola alisema: "Unataka vita? Sasa tunapigana

"Gabriel alisema vyema kwenye vyombo vya habari baada ya mechi, kwa hivyo hii ni vita. Tunapaswa kuwachochea wapinzani, kuwapa shinikizo…"

Beki wa kati wa Brazil Gabriel alisema baada ya mchezo huo: "Ni vita, vita, hivyo ni kawaida kuwa na vitendo vya uchochezi katika soka, ni sehemu ya mchezo. Sasa haya yameisha na tunawasubiri kwenye uwanja wetu."

Soma zaidi:

Arteta alisema nini?

Siku ya Jumanne, kocha wa Arsenal Mikel Arteta aliulizwa kuhusu shutuma za kutumia 'muujiza'.

Akizungumzia miaka mitatu na nusu aliyokaa kama msaidizi wa Guardiola akiwa City hadi Desemba 2019, Mhispania huyo alisema: "Nilikuwa huko kwa miaka minne. Nina taarifa zote, kwa hivyo najua, niamini."

Katika majibu yake siku ya Ijumaa, Guardiola aliongeza: "Wakati mwingine Mikel anapaswa kuwa wazi zaidi kuhusu kile anachomaanisha.

"Alisema alikuwa hapa kwa miaka minne na anajua hasa kinachotokea hapa. Hiyo inaweza kuhusishwa na mchakato unaoendelea wa mashtaka 115, labda anataarifa anazojua kuhusu hilo? Au labda alikuwa na kitu, sijui ...?

"Natumai swali hili limeulizwa na anaweza kujibu kile anachomaanisha."

City wamesalia na wiki mbili kabla ya kusikilizwa kwa kesi ambayo inaangazia madai ya ukiukaji wa sheria 115 za kanuni za fedha za Ligi Kuu ya Uingereza.

Wote Guardiola na Arteta walikuwa wakizungumza kwa wakati mmoja Ijumaa alasiri na kocha wa Arsenal alijaribu kupuuza pendekezo lolote kuonyesha kuwa wanazozana.

“Nampenda, namheshimu na ninamkubali,” aliongeza. "Ninaifurahia timu yake na kila kitu anachofanya.

"Huu ni mchezo. Jambo moja muhimu ni taaluma yetu, lingine ni uhusiano wetu wa kibinafsi. Ikiwa uhusiano wetu uliharibiwa kwa sababu mmoja alitoka sare na mwingine akashinda, au [kwa sababu ya] mara ambazo wametushinda, nisingezungumza naye tena.

'Hisia zipo' - ugomvi unaochochewa na vita vya kuwania ubingwa

Ushindani wa City na Arsenal umekua mkali zaidi katika misimu miwili iliyopita.

Msimu wa 2022-23 Arsenal walikuwa mbele kwa pointi nane kileleni mwa Ligi ya Primia mwanzoni mwa mwezi wa Aprili, lakini walipoteza nafasi hiyo katika mfululizo wa michezo minne bila ushindi na hatimaye kumaliza nafasi ya pili, wakiwa nyuma ya City kwa pointi tano.

Msimu uliopita, Gunners pia walikuwa kileleni mwezi Aprili lakini wakawapisha City katika nafasi hiyo walipofungwa 2-0 nyumbani na Aston Villa na kuishia kumaliza pointi mbili nyuma, licha ya kushinda mechi zao sita za mwisho.

Makali ya sasa baina ya vilabu hivyo viwili yalionyeshwa mara baada ya bao la kusawazisha la City la dakika za lala salama mwishoni mwa juma, wakati Haaland aliporusha mpira kichwani mwa Gabriel, tukio ambalo wadadisi wengi waliona lilipaswa kumfanya Mnorwe huyo afungiwe.

"Ningesema kwamba wakati mwingine hisia ziko," Guardiola aliongeza. "Nina hakika kabisa [Haaland] hana kiburi, lakini angalia, aina ya changamoto za Arsenal, naelewa."

Arsenal wanatarajiwa kucheza na City tarehe 1 Februari katika Ligi ya Primia, ingawa kuna uwezekano wanaweza kukutana katika mojawapo ya michuano miwili ya kombe la nyumbani kabla ya hapo.

Pia unaweza kusoma:

Imefasiriwa na Asha Juma