Clara Luvanga: Mchezaji wa Tanzania na Al Nassr azungumzia kuhusu 'shujaa' Ronaldo na azma yake ya kuwa mchezaji bora Afrika - BBC News Swahili (original) (raw)

.

Chanzo cha picha, Alnassr FC

Maelezo ya picha, Mshambuliaji nyota wa Tanzania, Clara Luvanga, alifurahia msimu wa kwanza katika klabu ya Al Nassr huku klabu hiyo ikitwaa taji la pili mfululizo la Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudia.

Wakati michuano mipya ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudia itakapoanza Ijumaa, mshambuliaji wa Al Nassr ya Tanzania, Clara Luvanga atakuwa anatafuta kuendeleza pale alipoachia.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 aliamua kuondoka Uhispania na kwenda Saudi Arabia Oktoba mwaka jana, licha ya uamuzi wake kuibua hisia chache, haswa katika nchi mwake.

Lakini tangu alipohama, hajatazama nyuma.

Wakati kampeni mpya ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Saudia itakapoanza Ijumaa, mshambuliaji wa Al Nassr ya Saudia, Clara Luvanga atakuwa anatafuta kuendelea na pale alipoachia.

"Ulikuwa msimu wangu bora hadi sasa na nina furaha sana kuisaidia timu [Al Nassr] kushinda ubingwa wao wa pili wa ligi," Luvanga aliambia BBC Sport Africa.

Miezi miwili tu kabla ya kujiunga na Al Nassr, Luvanga alikuwa amepewa fursa ya kujiunga na klabu ya daraja la pili ya Dux Logrono iliomsajili kutoka Yanga Princess ya Tanzania. Ilionekana kuwa mahali pazuri pa kukuza kipaji chake.

Hata hivyo, kijana huyo mwenye kipaji alicheza mechi sita pekee, akifunga mabao mawili, kabla ya Al Nassr - ambayo timu yake ya wanaume inawashirikisha Cristiano Ronaldo na Sadio Mane - kuharakisha kumleta Luvanga kwenye Ligi Kuu ya Wanawake ya Ufalme huo ilio changa.

Juhudi zake za kwanza zilizalisha mabao 11 na asisti saba – ikiwa ni asisti nyingi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote.

Ni wachezaji watatu pekee kwenye kitengo hicho waliofunga zaidi ya Luvanga - mmoja wao alikuwa mchezaji wa Algeria, kiungo wa zamani wa PSG Lina Boussaha.

Luvanga na Boussaha walikuwa tishio kubwa katika safu ya mashambulizi na kwa pamoja waliisaidia Al Nassr kutwaa taji la pili mfululizo.

"Nilikuwa na wakati mzuri sana nchini Uhispania lakini nilipopata fursa ya kwenda kucheza ligi ya Saudia, niliona ni bora kuangalia changamoto zingine kulingana na malengo yangu."

Mwaka 2022-23, ambao ndio msimu wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake, klabu hiyo ilishinda ubingwa kwa alama tatu; msimu uliopita, Nassr ilishinda kwa alama 10.

"Awali ilikuwa vigumu kuzoea mazingira ya Saudi Arabia, ikiwa ni pamoja na lugha, chakula na mambo mengi - lakini sasa nimezoea, na kila kitu kinaendelea vyema, na nina furaha."

Unaweza Pia Kusoma

Kuonana na Christiano Ronaldo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo na Sadio Mane wanacheza pamoja katika timu ya wanaume ya Al Nassr

Kuichezea Al Nassr kunamweka Luvanga kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia huko Riyadh.

Nyota wa Ureno Ronaldo alikuwa mfungaji bora wa klabu la Nassr - na wa ligi ya Saudi Pro League msimu uliopita huku Nassr ikimaliza wa pili nyuma ya mabingwa Al Hilal.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid anasaidiwa vyema katika safu ya mashambulizi katika klabu ya Nassr na mshambulizi bora wa muda wote wa Senegal Sadio Mane, wakati mshindi wa Euro 2024 Aymeric Laporte na kiungo wa zamani wa Inter Milan Marcelo Brozovic pia wakiichezea timu hiyo.

"Cristiano Ronaldo ni shujaa wangu katika soka ya wanaume," anasema Luvanga, ambaye pia anafichua kwamba Barbra Banda wa Zambia ni miongoni mwa mifano yake ya kuigwa katika soka. "Nimekuwa na bahati ya kumuona [Ronaldo] lakini bado sijakutana na Mane - natumai hilo linaweza kutokea hivi karibuni."

'Ni mchezaji mwenza mwenye kipaji na anayejua kucheza densi'

Luvanga, anayemungazia mchezaji wa kimataifa wa Tunisia Ghada Ayadi kama mmoja wa marafiki zake wa karibu katika chumba cha kubadilishia nguo, anasisitiza kuwa "nidhamu" ndio kitu muhimu kilichodhihirishwa na Al Nassr walipokuwa wakitetea ubingwa wao .

Fowadi huyo wa Tanzania alichangia pakubwa katika mafanikio hayo, huku mlinda lango wa Al Nassr na Saudi Arabia Sara Khalid Al-Dossary akisifu mchango wa Luvanga.

"Clara ni mchezaji mzuri na mchezaji mwenza wa kustaajabisha," Al-Dossary aliambia BBC Sport Africa. "Yeye ni mcheshi, ni dansa mzuri na anajitolea sana uwanjani.

"Yeye hujikosoa mwenyewe , wakati mwingine; ataingia na kuhisi kama angeweza kufanya zaidi au angefunga zaidi.

"Unaweza kuona anajisumbua lakini ni mchezaji mzuri ambaye anajitolea kwa kila kitu kwa timu na kwa wachezaji wanaomzunguka. Ninampenda tu.”

Jitihada za 'kuwa mchezaji bora barani Afrika'

.

Chanzo cha picha, Alnassr F.C.

Maelezo ya picha, Akiwa amefunga mabao 11 na kutoa asisti saba katika msimu wake wa kwanza akiwa na Al Nassr, Luvanga anatumai kuendeleza kiwango hicho katika Ligi ya Mabingwa ya Asia na Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake mwakani.

Timu ya wanawake ya Al Nassr ilifanikiwa wakati ambapo wanaume walishindwa msimu uliopita kushinda taji la nyumbani.

Ushindi huo wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudia unampa Luvanga na wachezaji wenzake fursa ya kushiriki katika Ligi ya Mabingwa ya Wanawake ya AFC iliyoanzishwa hivi karibuni - mashindano ya Asia, yaliyoboreshwa na ya klabu bingwa - mwaka 2024-25.

Nassr lazima kwanza ipitie mchujo, ambao unashirikisha mashindano madogo yanayochezwa Saudi Arabia kuanzia tarehe 25 Agosti, huku wapinzani wao watatu wakipangwa kuwa Abu Dhabi CC ya UAE, Myawady ya Myanmar na Young Elephants ya Laos.

"Ninafuraha sana kwamba nitacheza katika mashindano makubwa kama haya na ninaamini tutafanya vyema ikiwa tutaendelea kushirikiana kama timu," Luvanga anasema.

“Binafsi, nataka kuendelea kucheza kwa kiwango kizuri wakati wote na hatimaye nataka kuwa mchezaji bora zaidi barani Afrika na duniani kote.

Ili kufanya hivyo, unahitaji kucheza vyema katika mashindano makubwa kama [AFC] Ligi ya Mabingwa ya Wanawake."

Michuano mingine mikubwa inayolengwa na Luvanga ni Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake la CAF 2024 (Afcon).

Michuano hiyo ya bara Afrika ilipaswa kufanyika nchini Morocco mwaka huu lakini baada ya majaribio ya mara kwa mara haikufanyika, huku CAF ikithibitisha mwezi uliopita kuwa itafanyika kuanzia Julai 5-26, 2025.

Luvanga, ambaye alikuwa mfungaji bora wa CAF wakati wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake wasiozidi umri wa miaka 17 2022 akiwa na mabao kumi, anasisitiza kuwa hana wasiwasi na hana haraka huku akitarajia kutumia kipaji chake kuboresha matokeo ya kimataifa akiwa na Tanzania katika michuano hiyo ya mataifa 12 katika msimu ujao wa kiangazi.

"Ninahisi shinikizo lakini pia furaha kila wakati ninapochezea taifa langu," Luvanga anasema.

"Sijasikitishwa sana na kupangwa upya kwa Afcon - kusema kweli inanipa muda wa kujiandaa vyema.

"Natarajia kuwa na uzoefu wa kucheza Afcon na kupata nafasi ya kulipigania tena taifa langu."

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah