Leteni watoto wenye ulemavu wapate elimu (original) (raw)

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kuacha tabia ya kuwaficha na kuwanyima fursa muhimu ya kupata elimu.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kondoa mara baada ya kutembelea Shule ya Msingi Iboni inayojumuisha watoto wenye mahitaji maalumu akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo.

Amesema licha ya serikali kujenga miundombinu ikiwemo mabweni na madarasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu bado idadi ya watoto hao imeendelea kuwa ndogo katika vituo vya kutolea elimu.

Ametoa mfano katika Wilaya hiyo ya Kondoa, watoto 30 pekee wenye mahitaji maalumu ndio wamepelekwa katika shule ya Iboni wakati shule hiyo ina uwezo wa kupokea wanafunzi 200.

Makamu wa Rais amesema kitaaluma watoto wenye mahitaji maalumu wana uwezo mkubwa pamoja na vipaji. Amewahimiza viongozi wa serikali, dini, vyama na wananchi kutoa msisitizo wa kuwatafuta watoto wenye mahitaji maalumu waliopo majumbani na kuhakikisha wanapelekwa kupata elimu.

Dkt. Mpango amekabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule hiyo ikiwemo magodoro, viti mwendo, vyakula pamoja na vinywaji.

Shule ya Iboni inayojumuisha watoto wenye mahitaji maalumu imekamilisha mradi wa ujenzi wa mabweni mawili ambao umegharimu shilingi milioni 270.9.

Mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kusafiri umbali mrefu wa kutoka nyumbani kwenda shuleni.

Mradi huo pia utapunguza changamoto ya wanafunzi kutokufika shule kwa wakati pamoja na kuchangia kuweka mazingira bora na salama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi ya siku nne katika mkoa wa Dodoma.